Mark 6

Nabii Hana Heshima Kwao

(Mathayo 13:53-58; Luka 4:16-30)

1 aIsa akaondoka huko na kwenda mji wa kwao, akiwa amefuatana na wanafunzi wake. 2 bIlipofika siku ya Sabato, akaanza kufundisha katika sinagogi, na wengi waliomsikia wakashangaa.

Nao wakauliza, “Mtu huyu ameyapata wapi mambo haya yote? Tazama ni hekima ya namna gani hii aliyopewa? Tazama matendo ya miujiza ayafanyayo kwa mikono yake!
3 cHuyu si yule seremala, mwana wa Mariamu? Na ndugu zake si Yakobo, Yose,
Yusufu kwa Kiyunani ni Joses.
Yuda na Simoni? Dada zake wote si tuko nao hapa kwetu?” Nao wakachukizwa sana kwa ajili yake, wakakataa kumwamini.

4 eIsa akawaambia, “Nabii hakosi heshima isipokuwa katika mji wake mwenyewe, na miongoni mwa jamaa na ndugu zake, na nyumbani kwake.” 5 fHakufanya miujiza yoyote huko isipokuwa kuweka mikono yake juu ya wagonjwa wachache na kuwaponya. 6 gNaye akashangazwa sana kwa jinsi wasivyokuwa na imani.

Isa Awatuma Wale Kumi Na Wawili

(Mathayo 10:5-15; Luka 9:1-6)

Kisha Isa akawa anakwenda kutoka kijiji kimoja hadi kingine akifundisha.
7 hAkawaita wale kumi na wawili, akawatuma wawili wawili, na kuwapa mamlaka kutoa pepo wachafu.

8Akawaagiza akisema, “Msichukue chochote kwa ajili ya safari isipokuwa fimbo tu. Msichukue mkate, wala mkoba, wala fedha kwenye mikanda yenu. 9 iVaeni viatu, lakini msivae nguo ya ziada.” 10 jAkawaambia, “Mkiingia kwenye nyumba yoyote, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo. 11 kKama mahali popote hawatawakaribisha wala kuwasikiliza, mtakapoondoka huko, kung’uteni mavumbi kutoka kwenye miguu yenu ili kuwa ushuhuda dhidi yao.”

12 lKwa hiyo wakatoka na kuhubiri kwamba inawapasa watu kutubu na kuacha dhambi. 13 mWakatoa pepo wachafu wengi, wakawapaka wagonjwa wengi mafuta na kuwaponya.

Yahya Mbatizaji Akatwa Kichwa

(Mathayo 14:1-12; Luka 9:7-9)

14 nMfalme Herode akasikia habari hizi, kwa maana jina la Isa lilikuwa limejulikana sana. Watu wengine walikuwa wakisema, “Yahya Mbatizaji amefufuliwa kutoka kwa wafu, ndiyo sababu nguvu za kutenda miujiza zinafanya kazi ndani yake.”

15 oWengine wakasema, “Yeye ni Ilya.”

Nao wengine wakasema, “Yeye ni nabii, kama mmojawapo wa wale manabii wa zamani.”

16 pLakini Herode aliposikia habari hizi, akasema, “Huyo ni Yahya Mbatizaji, niliyemkata kichwa, amefufuliwa kutoka kwa wafu!”

17 qKwa kuwa Herode alikuwa ameagiza kwamba Yahya Mbatizaji akamatwe, afungwe na kutiwa gerezani. Alifanya hivi kwa sababu ya Herodia, mke wa Filipo, ndugu yake, ambaye Herode alikuwa amemwoa. 18 rYahya alikuwa amemwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa ndugu yako.” 19Kwa hiyo Herodia alikuwa amemwekea Yahya kinyongo akataka kumuua. Lakini hakuweza, 20 skwa sababu Herode alimwogopa Yahya akijua kwamba ni mtu mwenye haki na mtakatifu, hivyo akamlinda. Herode alifadhaika sana alipomsikia Yahya, lakini bado alipenda kumsikiliza.

21 tMfalme Herode alifanya karamu kubwa wakati wa sikukuu ya kuzaliwa kwake. Akawaalika maafisa wake wakuu, majemadari wa jeshi na watu mashuhuri wa Galilaya. Hatimaye Herodia alipata wasaa aliokuwa akiutafuta. 22Binti yake Herodia alipoingia na kucheza, akamfurahisha Herode pamoja na wageni wake walioalikwa chakulani.

Mfalme Herode akamwambia yule binti, “Niombe kitu chochote utakacho, nami nitakupa.”
23 uTena akamwahidi kwa kiapo, akamwambia, “Chochote utakachoomba nitakupa, hata kama ni nusu ya ufalme wangu.”

24Yule binti akatoka nje, akaenda kumuuliza mama yake, “Niombe nini?”

Mama yake akamjibu, “Omba kichwa cha Yahya Mbatizaji.”

25Yule binti akarudi haraka kwa mfalme, akamwambia, “Nataka unipe sasa hivi kichwa cha Yahya Mbatizaji kwenye sinia.”

26 vMfalme akasikitika sana, lakini kwa sababu alikuwa ameapa viapo mbele ya wageni wake, hakutaka kumkatalia. 27Mara mfalme akatuma askari mmojawapo wa walinzi wake kukileta kichwa cha Yahya. Akaenda na kumkata Yahya kichwa humo gerezani, 28akakileta kichwa chake kwenye sinia na kumpa yule msichana, naye yule msichana akampa mama yake. 29Wanafunzi wa Yahya walipopata habari hizi, wakaja na kuuchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

Isa Awalisha Wanaume 5,000

(Mathayo 14:13-21; Luka 9:10-17; Yohana 6:1-14)

30 wWale mitume wakakusanyika kwa Isa na kumpa taarifa ya mambo yote waliyokuwa wamefanya na kufundisha. 31 xBasi kwa kuwa watu wengi mno walikuwa wakija na kutoka, hata wakawa hawana nafasi ya kula, Isa akawaambia wanafunzi wake, “Twendeni peke yetu mahali pa faragha, mpate kupumzika.”

32 yHivyo wakaondoka kwa mashua peke yao, wakaenda mahali pasipo na watu. 33Lakini watu wengi waliowaona wakiondoka, wakawatambua, nao wakaenda haraka kwa miguu kutoka miji yote, nao wakatangulia kufika. 34 zIsa alipofika kando ya bahari, aliona makutano makubwa ya watu, akawahurumia kwa maana walikuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji. Kwa hiyo akaanza kuwafundisha mambo mengi.

35 aaMchana ulipokuwa umeendelea sana, wanafunzi wake walienda kwake, wakamwambia, “Mahali hapa ni nyikani, nazo saa zimekwenda sana. 36Waage watu ili waende mashambani na vijijini jirani, wakajinunulie chakula.”

37 abLakini Isa akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wakamwambia, “Je, twende tukanunue mikate ya dinari 200
Dinari moja ilikuwa kama mshahara wa kibarua wa siku moja; hivyo dinari 200 ni sawa na mshahara wa siku 200.
ili tuwape watu hawa wale?”

38 adAkawauliza, “Kuna mikate mingapi? Nendeni mkaangalie.”

Walipokwisha kujua wakarudi, wakamwambia, “Kuna mikate mitano na samaki wawili.”

39Kisha Isa akawaamuru wawaketishe watu makundi makundi kwenye majani, 40nao wakaketi kwenye makundi ya watu mia mia na wengine hamsini hamsini. 41 aeIsa akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akainua macho yake akatazama mbinguni, akavibariki na kuimega ile mikate. Kisha akawapa wanafunzi wake ili wawagawie wale watu wote. Pia akawagawia wote wale samaki wawili. 42Watu wote wakala, wakashiba. 43 afNao wanafunzi wake wakakusanya vipande vilivyosalia vya mikate na samaki, wakajaza vikapu kumi na viwili. 44Idadi ya wanaume waliokula walikuwa 5,000.

Isa Atembea Juu Ya Maji

(Mathayo 14:22-33; Yohana 6:15-21)

45 agMara Isa akawaambia wanafunzi wake waingie kwenye mashua watangulie kwenda Bethsaida, wakati yeye alikuwa akiwaaga wale makutano. 46 ahBaada ya kuwaaga wale watu, akaenda mlimani kuomba.

47 aiIlipofika jioni, ile mashua ilikuwa imefika katikati ya bahari, na Isa alikuwa peke yake katika nchi kavu. 48 ajAkawaona wanafunzi wake wanahangaika na kupiga makasia kwa nguvu, kwa sababu upepo ulikuwa wa mbisho. Wakati wa zamu ya nne ya usiku, Isa akawaendea wanafunzi wake, akiwa anatembea juu ya maji. Alikuwa karibu kuwapita, 49 aklakini walipomwona akitembea juu ya maji, wakadhani ni mzimu. Wakapiga yowe, 50 alkwa sababu wote walipomwona waliogopa.

Mara Isa akasema nao, akawaambia, “Jipeni moyo! Ni mimi. Msiogope!”
51 amAkapanda ndani ya mashua nao, na ule upepo ukakoma! Wakashangaa kabisa, 52 ankwa kuwa walikuwa hawajaelewa kuhusu ile mikate. Mioyo yao ilikuwa migumu.

53 aoWalipokwisha kuvuka, wakafika nchi ya Genesareti, wakatia nanga. 54Mara waliposhuka kutoka mashua yao, watu wakamtambua Isa. 55Wakaenda katika vijiji vyote upesi, wakawabeba wagonjwa kwenye mikeka ili kuwapeleka mahali popote waliposikia kuwa Isa yupo. 56 apKila mahali Isa alipokwenda, iwe vijijini, mijini au mashambani, watu waliwaweka wagonjwa wao masokoni. Wakamwomba awaruhusu hao wagonjwa waguse japo upindo wa vazi lake. Nao wote waliomgusa waliponywa.
Copyright information for SwhKC